Mkwamo na mvutano ungali unaendelea kwa siku ya pili mfululizo kati ya wafuasi wa Khan na maafisa wa vyombo vya sheria karibu na makazi ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan mjini Lahore.
Polisi kutoka mji mkuu Islamabad wanajaribu kumkamata Khan katika kesi inayohusu kuuza zawadi za serikali zilizotolewa na viongozi wa kigeni alipokuwa waziri mkuu.
Chama cha Imran Khan Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kimesema katika jumbe kilizotuma kwenye mitandao ya kijamii kwamba polisi wameanza tena kufyatua mabomu ya kutoa machozi nje ya makazi yake ya Zaman Park huko Lahore.
Katika ujumbe aliotuma kwa njia ya video, waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan aliyeuzuliwa na bunge amesisitiza kuwa, yuko tayari kutoa dhamana na hakikisho kwamba atafika mahakamani siku ya Jumamosi ili kupanda kizimbani katika kesi inayomkabili.
Mahakama ya chini katika mji mkuu Islamabad ilitoa hati ya kukamatwa Khan kwa kutofika mbele yake licha ya kuitwa mara kadhaa. Khan anatuhumiwa kuuza zawadi hizo za serikali kinyume cha sheria akiwa madarakani kuanzia 2018 hadi 2022, lakini anakanusha kutenda kosa hilo.
Katika hotuba yake mapema leo, waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan amesema kulikuwa na wasiwasi wa kiusalama katika mahakama ambayo alipaswa kufika mbele yake mjini Islamabad kwa sababu hapo awali yalishafanywa mashambulizi mawili na wanamgambo katika eneo hilo.../
342/